Wednesday, September 19, 2012

WATOTO WATEMBEA KM 15 KUFUATA SHULE

Na,Jumbe Ismailly
 
Ikungi, Singida     


WANAFUNZI wa shule ya awali ya Kijiji cha Damaida,kata ya Mkiwa,wilaya mpya ya Ikungi hutembea umbali wa kilomita 15 kwenda na kurudi kufuata masomo yao katika shule hiyo.

Hayo yamebainishwa na mmoja wa walimu wa shule hiyo,Sister Maria Mwiru alipokuwa akitoa maelezo mafupi ya shule hiyo kwa mkuu wa wilaya hiyo,Bwana Manju Msambya aliyetembelea shule hiyo kuona changamoto zinazoikabili shule hiyo.
Amefafanua mwalimu huyo kuwa mahudhurio ya katika shule hiyo yenye wanafunzi sitini wenye umri wa kati ya miaka 3 hadi 5 ni mazuri sana wakati wa kiangazi lakini yamekuwa mabaya pia katika kipindi cha masika kutokana na watoto hao wadogo kushindwa kutembea umbali huo.
 
Kwa mujibu wa Sir Mwiru kiwango cha mahudhurio wakati wa kiangazi hufikia asilimia mia moja lakini kwa kipndi cha masika hushuka hadi kufikia asilimia hamsini kutokana na wanafunzi kushindwa kutembea kwenye udongo wenye tope la kunata sana.
Ili kukabiliana na changamoto hiyo,mwalimu huyo wa shule hiyo inayomilikiwa na Wamishenari wa Urusula Mkiwa ameweka wazi kuwa walilazimika kutofunga shule mwezi wa nane ili waweze kusogeza silabasi kabla ya mvua za masika hazijaanza kunyesha.
Hata hivyo Sir Mwiru ameweka bayana baadhi ya changamoto wanazokabiliana nazo kuwa ni kwamba kutokana na wanafunzi wanaosoma katika shule hiyo ni watoto wa wafugaji wa jamii ya kabila la kisukuma hivyo wamekuwa wakijaribu kwenda kuwafuata nyumbani kwao na kuwashauri watoto wa wafugaji hao ili waweze kwenda shule.
Aidha mwalimu Mwiru amesisitiza pia kwamba wanapokwama baada ya kutoa ushauri kwa wazazi wa wanafunzi hao ndipo hulazimika kuwatumia askari wa jeshi la mgambo kwenda kuwafuata na kuwatisha tu ila bila kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria ili waweze kuhudhuria masomo,jambo ambalo amesema limeleta mafanikio makubwa sana ya mahudhurio.
Shule ya awali Damaida licha ya kutoa huduma ya masomo kwa watoto hao wenye umri wa kati ya miaka 3 hadi 5,vile vile hutoa chakula cha mchana kwa wanafunzi wote wanahudhuria masomo,kitendo ambacho kimesaidia pia ongezeko la mahudhuria ya shule hiyo.

No comments: