HALIMA JAMAL
SINGIDA
Watu 9 wamekufa papohapo na wengine
25 kujeruhiwa baada ya ajali mbili tofauti kutokea mkoani singida leo asubuhi.
Taarifa za awali kutoka kwa Kamanda
wa polisi mkoani Singida Linus Sinzumwa zimeeleza kuwa gari la kwanza kutokea
ajali kuwa ni PT1149 aina ya land rover mali ya Polisi mkoani Morogoro na gari
ya pili kuwa ni T126 AU aina ya fuso iliyokuwa ikitokea Singida mjini kuelekea
kijiji cha mtavira kwa ajili ya mnada.
Alisema ajali ya kwanza iliyohusisha
gari ya polisi,ilikuwa ikisafirisha maiti ya askari polisi kutokea Morogoro
kwenda Musoma ikiwa imebeba watu kumi na moja.
Aidha alisema gari hiyo ilipofika
maeneo ya nje kidogo ya mji wa singida ijulikanayo kama kambi ya wachina
iliacha njia na kuanza kubiringita na kusababisha vifo vya watu wanne papo
hapo.
Sinzumwa alisema kuwa baada ya
kupata taarifa hiyo baada ya dakika kadhaa aliweza kupata tena taarifa ya kuwa
kuna ajali nyingine tena imetokea maeneo ya Minyughe.
Alisema baada ya kutuma askari wake kwenye
eneo la tukio ndipo walikuta gari aina ya fuso iliyokuwa ikielekea mnadani
imepinduka na kukuta maiti za watu watano na majeruhi ndipo walipowachukua na
kuwakimbiza hospitali ya mkoa.
Aidha Sinzumwa aliwataja waliokufa
katika ajali ya gari la polisi kuwa ni Rehema Juma,Regu Kamamo,Rosemary
Nyabuzuki pamoja na mmoja aliyefanamika kwa jina moja tu la Juma.
Sinzumwa aliwataja waliokufa kwenye
ajali ya fuso kuwa ni Sarafina Ally,Mtalika Bilali ,Charles Thomas,Bakari
pamoja na Pili Saidi.
Maulidi Mohamedi ambaye ni majeruhi
wa ajali ya fuso amesema kuwa ajali hiyo imetokana na breki za gari hilo kufeli
likiwa linateremsha mlima mkali na dereva wa gari hilo kushindwa kulimudu na
kusababisha kuacha njia na kupinduka.
''Bado tunaendelea zaidi na
uchunguzi wa ajali zote mbili tukikamilisha tutawaita ili muweze kuwa na
uhakika nini chanzo zaidi ya ajali hizo''alisema Sinzumwa.
Aidha kamanda alisema kuwa majeruhi
wa ajali zote wanaendelea kupata matibabu katika hospitali ya mkoa na kuwa hali
zao zinaendelea vizuri.
Sinzumwa ametoa wito kwa madereva
kuwa makini barabarani kwani roho za watu wengi zinapotea kwa uzembe wa watu
wachache.
No comments:
Post a Comment