Sunday, September 9, 2012

WANA HABARI IRINGA WAMLILIA MWANGOSI

Na. Frank Leonard
Iringa
 
It's too painful for me to think of Daudi lying like a piece of meat in a butcher so I cant console myself.

Machozi yananitoka Mwangosi si tu kwasababu umekufa, lakini kwasababu umekufa kinyama mbele ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, kwangu mimi nimepoteza mtu wa jirani, ndugu na rafiki yangu mpendwa, hakika hukustahili kifo cha kinyama namna ile.

Umekufa ukitimiza wajibu wako wa kutaka kuwahabarisha watanzania kile kilichokuwa kinajili katika kijiji cha Nyololo. Kamera yako ilibeba picha nyingi zikiwemo zile zilizokuwa zikionesha jinsi askari walivyokuwa wakifyatua mabomu ya machozi kwa wananchi wasio na hatia.Mwangosi huenda kazi yako iliwatisha zaidi Polisi baada ya kuona wanachokifanya hakiendani na dhamira halisi ya kutiliza ghasia.

Kwasababu ulitaka kuonesha upuuzi wao ndiyo maana hata RPC Michael Kamuhanda alipoombwa na mwandishi mwingine wa habari akusaidie ili askari wale wasiendelee kukupiga, hakuthubutu kuinua mkono au redio call yake kuwaamuru wakuache.

Mwangosi wapo watu waliokuwepo kwenye tukio na ambao hawakuwepo kwenye tukio wamekuja na kauli za ajabu wengine wakisema ulikuwa na bomu mfukoni na wengine wakisema ulirushiwa kitu kizito kutoka kwa wafuasi wa Chadema wakati ukitafuta msaada wa Polisi. Kauli hizi ndugu yangu Mwangosi zimekuwa zikitolewa huku wengi katika utawala huu ambao tunadhani ni marafiki zetu kwasababu tunafanya nao kazi za kila siku mbali na kushindwa kusema neno moja tu 'POLENI' kwa jamaa zako uliotuacha, wala hawakutaka kujua msiba wako uko wapi.

Mwangosi taarifa hizi ambazo jeshi la Polisi linataka kuzitumia kupotosha ukweli wa tukio, hakika hazikubaliki na wanaofanya hivyo ipo siku, kifo chako kitakuja kuwaumbua, leo wanataka kujifanya wanataarifa za kweli ili kulifurahisha jeshi la Polisi na watawala, nachoamini mimi ni kwamba Damu yako iliyomwagika kwa makusudi wakati ukitimiza wajibu wako haitapotea bure na wanaoingia katika mtego wa kutoa taarifa za kupotosha watahukumiwa kwa kifo chako.

Kuna uwezekano tume zinazofanya kazi zikaja na majibu tofauti na ushahidi wa picha za mnato, za video, waandishi wa habari na wananchi walioshuhudia tukio lile katika makaratasi yao na kuita ripoti ya uchunguzi, NAOMBA NIKUHAKIKISHIE WAANDISHI WA HABARI NA UMMA WA WATANZANIA KWA KIASI KIKUBWA UPO NYUMA YAKO NA HAKI DHIDI YA UDHALIMU HUO ITAPATIKANA.

Majira ya saa 4 asubuhi ya Septemba 2, ilikuwa siku ya mwisho kwangu kuisikia sauti yako baada ya mimi na wewe kuongea kwa njia ya simu nikikutaarifu ufuatilie taarifa ya kuwepo kwa mchungaji shoga katika moja ya makanisa ya mjini Iringa. Wakati huo mimi nilikuwa stendi kuu nikitafuta usafiri kwa ajili ya safari yangu ya kwenda Dar es Salaama na ambayo nawe ulikuwa una taarifa nayo.

Wakati nikikuaga, tulikubaliana kwamba tutakutana Dar es Salaam ambako kwa pamoja ilikuwa tushiriki mkutano mkuu wa UTPC uliofanyika Septemba 6 na 7, mwaka huu. Lakini haikuwa kama ilivyokuwa katika ratiba yetu na badala ya mimi kukusubiri Dar es Salaam, nililazimika kurudi Iringa ili kujumuika na watanzania wengine kuomboleza kifo chako japokuwa sikuwa mazishi yako.

Sitaisahau Septemba 1, 2012 katika maisha yangu yote, kwani ndiyo siku ya mwisho kwangu mimi na wewe kukutana uso kwa uso na kama kawaida yetu kukaaa pamoja.

Mara baada ya kumaliza mkutano mkuu wa IPC, siku hiyo tulifanya get together party na baada ya wanachama wote kuondoka mimi na wewe tulikuwa wa mwisho kufungasha vilago. Ilikuwa majira ya saa sita usiku, mimi nikikuaga kwamba naenda nyumbani ili nikajiandae na safari na wewe ukinishauri twende disco tukafurahi hata kwa saa moja.

Nilikataa na nikatoa vifaa vyako vya kazi vilivyokuwa ndani ya gari yangu, nikakukabidhi na kukuacha sehemu tuliyokuwa tumefanyia party yetu ukimalizia ulichokuwa umeacha mezani tayari kwa kwenda Disco.

Mwangosi, IPC na waandishi wa habari wote mkoani Iringa watakukumbuka kwa ujasiri wako katika kuyasimamia mambo uliyoyaamini ikiwa ni pamoja na utetezi wa haki za waandishi, misimamo, mitizamo, ucheshi na tabia ya kupenda kujifunza wakati ukijisomea vitabu mbalimbali kwa lengo la kuongeza maarifa yako.

Septemba 2, imeingia katika historia ya nchi na ya dunia hii, kwasababu tukio ulilofanyiwa na askari hao ambao wanadhani katika maisha yao yote wataendelea kuwa askari wa kawaida na wenye vyeo huku wakiishi katika kambi na nyumba za jeshi hilo, halikuwahi kutokea hapa nchini mpaka lilipotokea kwako.

Kwetu sisi wanahabari, Septemba 2 tutaifanya siku maalumu. Itakuwa siku ya kumkumbuka shujaa wetu, hakika umetuacha japokuwa wote njia yetu ni moja lakini tunakuhakikishia silaha ulizoziacha tunazibeba na kwa nguvu zetu zote tutaendelea kuitumikia jamii ili ijue mabaya na mazuri yanayotokea ndani ya nchi hii.

MUNGU AILAZE ROHO YAKO MAHALI PEMA PEPONI. AMIN

No comments: