Na HALIMA JAMAL
Singida
MKUU wa mkoa wa Singida,Dk.Parseko Kone, amewataka waandishi wa habari mkoani hapa kuanzisha kikundi cha kuweka na kukopa (SACCOS),ili kujijengea mazingira mazuri ya kukopesheka.
Dk.Kone ametoa changamoto hiyo wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye viwanja vya ofisi yake juzi.
Alisema maisha ya kutegemea mishahara au posho peke yake,uzoefu unaonyesha kuwa maisha hayo kamwe hayawezi kukidhi mahitaji yote muhimu.
Dk.Kone alisema dawa pekee ya kumaliza makali ya maisha, ni kujiunga/kuanzisha SACCOS mahali mikopo ya masharti nafuu,inapatikana.
“Mkianzisha SACCOS yenu,mtavutia taasisi mbalimbali za kifedha kuweza kuwakopesha fedha.Fedha hizo mtazitumia katika kukopeshana kwa ajili ya kuendesha miradi mtakayoianzisha ya kuwaingizia kipato”,alisema mkuu huyo wa mkoa.
Akiijengea nguvu hoja yake hiyo, aliwataka waige mifano kutoka kwa wafanyakazi wa idara za serikali,makampuni na asasi mbalimbali ambao wameboresha hali zao za kiuchuni kupitia SACCOS zao.
“Chukueni mfano kutoka kwa wafanyakazi wa ofisi yangu wanavyoneemeka na SACCOS yao,sio ofisi yangu tu,hata wafanyakazi wa benki kuu nao wana SACCOS yao.Wafanyakazi wa benki kuu kwa vyo vyote mishahara yao ni mikubwa pengine kuliko yenu.Lakini pamoja na mishahara yao hiyo, wana SACCOS ambayo inawasaidia kujiendeleza kiuchumi”,alifafanua.
Aidha Dk.Kone alisema anaamini kwamba waandishi wa habari wakiwa na hali nzuri kiuchumi,watatekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.
Aidha,alisema anaamini pia kwamba waandishi wa habari hali zao za kiuchumi zikiwa nzuri,mkakati wa kukuza uhuru wa vyombo vya habari na kuhakikisha viwango vya juu kabisa vya weledi na uwajibikaji,utafanikiwa.
“ kweli,niko ‘serious’ na jambo hili,nataka nitakapoondoka mkoani Singida, niache kila mwandishi wa habari,anakuwa na hali ya kuridhisha ya kiuchumi”,aliongeza Kone.
“Ni kupitia SACCOS pekee ndio mtaweza kujijengea nyumba bora,kugharamia masomo ya watoto wenu na mambo mengine yote muhimu kwa maisha”.
Kwa upande wake katibu msaidizi wa klabu ya waandishi wa habari (Singpress) mkoa wa Singida,Emmanuel Michael,alimhakikishia mkuu huyo wa mkoa Dk.Kone,kuwa ushauri wake huo wataufanyia kazi mapema iwezekanavyo.
“Kwa kweli hali zetu za kiuchumi haziridhishi kabisa.Kwa kifupi wengi wetu tumepigika kimaisha.Mbaya zaidi ni kwamba tumekuwa tukitumia kalamu zetu katika kuyahamasisha makundi mengine kujikomboa kiuchumi huku sisi wenyewe tukijisahau”,alisema katibu huyo msaidizi.
Emmanuel ambaye ni mwandishi wa habari wa radio free afrika na star tv, alisema ushauri huo wataufanyia kazi ili wafike mahali hali zao za kiuchumi na pia klabu yao iwe na uwezo wa kujitegemea.
No comments:
Post a Comment