Na. Jumbe ismail na Everister Lucas
Singida
KATIBU wa Idara ya Utumishi wa
Walimu Mkoa wa Singida amewaasa vijana wanaomaliza masomo ya elimu ya kidato
cha nne nchini kujiepusha na maambukizi mapya ya ugonjwa wa Ukimwi kutokana na
kile alichodai kwamba dawa ya kutibu bado haijapatikana.
Katibu huyo,Bwana Samwel
Olesaitabahu ametoa tahadhari hiyo wakati wa sherehe za mahafali ya 11 ya
kidato cha nne katika shule ya sekondari Singida,iliyopo kwenye Manispaa ya
Singida.
Amefafanua Bwana Olesaitabahu kuwa
idadi kubwa ya vijana wanaomaliza elimu ya sekondari ya kidato cha nne na hata
kabla ya kumaliza masomo yao huanza kujingiza kwenye vitendo vya
uasherati,jambo ambalo amesema linachangia kwa kiasi kikubwa kupoteza nguvukazi
ya taifa.
Aidha afisa huyo mwenye dhamana ya
kusimamia idara ya utumishi ameweka wazi kuwa malevi kwa vijana ni jukumu la
wote kati ya wazazi na walimu,na kwamba ni dhana potofu kuwa walimu ndio wenye
majukumu ya kuwasimamia wanafunzi hao.
Hata hivyo afisa huyo amebainisha
kwamba ili kufanikisha kupata vijana wenye malezi mema ni vyema wazazi kwa
kushirikiana na walimu kuwalea kwa uangalifu wanafunzi na kwamba haitakuwa
vizuri kazi hiyo ikaachwa kwa walimu peke yao.
Kuhusu suala la nidhamu kwa
wanafunzi,Bwana Olesaitabahu amesema suala la nidhamu katika shule yeyote ile
ni la utatu kwa maana kwamba walimu,wanafunzi pamoja na uongozi wa shule,hauna
budi kuwa na nidhamu ya pamoja kwa lengo la kuleta ufanisi kwenye taaluma.
Hata hivyo akijibu risala ya
wanafunzi waliomaliza kidato cha nne katika shule hiyo,katibu huyo amesisitiza
kwamba uongozi wa shule hiyo hauna budi kuweka kipaumbele kulingana na
changamoto zinazowakabili wanafunzi wa shule hiyo.
Amefafanua huku akitoa mfano wa
vipaumbele katibu huyo wa idara ya utumishi aliutaja ujenzi wa uzio wa
kutenganisha chuo na shule hiyo ya sekondari.
Hata hivyo hakusita kuushauri
uongozi wa shule hiyo kuanza mara moja kuweka mikakati ya kuendeleza shule
hiyo,hususani ujenzi wa uzio huo na alitumia fursa hiyo kuwapongeza walimu
wanaofundisha shule binafsi licha ya walimu hao kufundishwa na serikali.
Awali katika risala yake,Mkuu wa
shule hiyo,Bwana Francis Ibabila amesema licha ya mafanikio yaliyopatikana
katika shule hiyo,lakini bado shule hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali
ikiwa ni kukosekana kwa maabara,maktaba pamoja na uzio unaotenganisha kati ya
chuo na shule ya sekondari hiyo.
Kwa mujibu wa mkuu huyo wa shule
kukosekana kwa uzio huo unachangia kwa namna moja au nyingine ukosefu wa
nidhamu kwa wanafunzi wanaosoma katika shule hiyo.
Changamoto zingine kwa mujibu wa
Bwana Ibabila ni upungufu wa maji ya kutosheleza mahitaji ya wanafunzi pamoja
na utoro wa wanafunzi unaosababishwa na ushirikiano mdogo kati ya walimu na
wazazi.
Katika
mahafali hayo ya 11 jumla ya vijana 56 wakiwemo wavulana 26 na wasichana 30
wamehitimu kidato cha nne katika shule ya sekondari Singida,iliyopo katika
Manispaa ya Singida.
No comments:
Post a Comment