Masuala ya Msingi
Katika Mwelekeo Mpya wa Hatima ya Taifa Letu
Na Gwandumi Gwappo
Atufwene Mwakatobe
Septemba 15, 2012, Mwakaleli (Kandete)
1. Itikadi na
Falsafa ya Taifa
Taifa
letu linapaswa kuwa na itikadi na falsafa inayotuongoza na inayoweza kurithishwa
kutoka vizazi vilivyopo na vijavyo. Itikadi na falsafa ambayo inalinda utamaduni
wetu, utu wetu na maisha yetu kwa kuyapa kipaumbele cha kwanza dhidi ya vitu na
mali. Itikadi na falsafa nyingi zilizopo na zilizopita zinalenga mifumo ya
uchumi badala ya kujikita katika kulinda heshima na hadhi ya utu wa mtu kwanza.
Tumepitia vipindi vya ujima, ujamaa, ubepari, ubeberu na mitazamo inayokinzana
kimrengo ambayo yote inahusiana na mali au utajiri wa kiuchumi (material
wealth), ambayo haijali utu na maisha ya mtu. Tumesahau kuuendeleza utu,
heshima na utukufu alionao mtu bila kujali matabaka ya maisha kiuchumi. Bila
itikadi na falsafa inayotuongoza tutakosa utamaduni wetu na tutakosa mwelekeo
wa jamii na taifa kwa ujumla.
Kwa
waraka huu natamka kwamba nchi yetu itafuata itikadi na falsafa ifuatayo:
Kulinda, Kuheshimu na Kuendeleza Misingi ya Utu wa
Mtu na Maisha Yake Kwanza Kuliko Mali na Vitu.
Misingi ya Utu ina mihimili
mikuu minne: Huruma, Ukarimu, Kujali na Utumishi wa
mtu kwa binadamu wenzake, hususan jamii inayomzunguka na taifa lake. Maliasili
au rasilimali zozote zile kama wanyamapori, misitu, maji, madini, fedha,
nakadhalika, haviwezi kupewa kipaumbele kuliko utu wa mtu na maisha yake.
2. Haki ya Msingi
ya Raia
Raia
yeyote nchini anayo haki ya kushiriki kikamilifu katika kuiendeleza jamii na
taifa kwa ujumla kwa kutumia kipaji, ujuzi, utaalamu, maarifa na nguvu
alizonazo bila kizuizi chochote. Haki ya kuitumikia na kuiendeleza jamii yako ndiyo
haki ya msingi na nguzo ya umoja wa kijamii na kitaifa. Ieleweke
kuwa hakuna jamii au nchi yoyote duniani iliyoendelezwa na taasisi au chama cha
siasa. Nchi inaendelezwa na raia wake wenye uzalendo na uchungu wa kimaendeleo
kwa kutumia tunu zao walizojaliwa na Mungu – si chama cha siasa. Mhandisi,
fundi, mbunifu, mkulima, msanii, mtaalamu wa tiba, mwalimu, mwanamichezo, mvuvi,
mjasiriamali, mwenye kipaji cha uongozi, nakadhalika; hao ndio huiendeleza nchi.
Ukiwa
mhandisi huhitaji kuwa mwanachama wa chama cha siasa ili kulijenga taifa lako.
Ukiwa mkulima stadi huhitaji kibali au tiketi ya chama cha siasa ili uinue
kilimo nchini. Vivyo hivyo ukiwa na kipaji cha uongozi huhitaji kuwa mwanachama
wa chama cha siasa ili kuiongoza jamii yetu katika ngazi yoyote ile, mathalani
uenyekiti wa kijiji, udiwani, ubunge na hata urais.
Haki
ya kiraia ya kutumia kipaji chako kuliendeleza taifa letu ni haki ya msingi
ambayo haipaswi kuwekewa kizuizi au sharti la aina yoyote ile. Ni ukandamizaji
usio mithilika kumtaka raia katika nchi yake apitie chama cha siasa ili awe
mkulima, mhandisi, mganga, mwalimu au kiongozi kwa kushika wadhifa au cheo
katika ngazi yoyote ile. Na kwa msingi huo hatusemi huyu ni mgombea binafsi
bali ni mgombea kupitia haki yake ya kiraia ilmradi amethibitika kuwa ni raia
wa Tanganyika, Zanzibar au Tanzania kwa mambo ambayo yanahusu muungano.
3. Kukomesha Ubaguzi
na Ukiritimba wa Vyama vya Siasa Ili kujenga Umoja
Vyama
vya siasa vimenyang’anya kwa muda mrefu haki ya uhuru na ushiriki wa wananchi
katika kujiletea maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kiutamduni. Tumekuwa
tukipiga kelele kwamba ukabila, rangi, udini na matabaka ya watu kimaisha yanaleta
ubaguzi na hata uhasama. Lakini vyama vya siasa vimekuwa vikifanya ubaguzi na
uhasama mkubwa zaidi na hata kuthubutu kudai serikali ni mali ya chama fulani,
wakati kiukweli inatokana na wananchi na ni taasisi ya umma – si chama cha
siasa. Chama kinapodai serikali ni mali yake wakati inawekwa madarakani na umma
huwafanyi watu wa vyama vingine na wasio na vyama wajisikie kwamba si serikali
yao. Wanaona hawana serikali, jambo ambalo tunaona wanaojiita wenye chama tawala wakipandisha mabega na
kujiona wana haki zaidi katika nchi kuliko wananchi wenzao. Ni ubaguzi mbaya
unaovunja umoja wetu wa kitaifa kudai serikali ni ya chama fulani. Serikali ni taasisi ya umma, si ya chama
cha siasa. Chama ni taasisi au asasi ya baadhi ya watu, si ya umma. Vyama vya
siasa vinakuja na kuondoka lakini taifa litadumu daima endapo umoja wa kitaifa utalindwa
na kuzingatiwa.
Katiba
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Toleo la 2008, Sehemu ya Pili, ibara ya 8,
kifungu cha 1(a), ukurasa wa 23, inabainisha wazi kwamba: “Wananchi ndio msingi wa mamlaka
yote, na serikali itapata madaraka na mamlaka yake kutoka kwa wananchi kwa
mujibu wa Katiba hii.” Serikali inapata madaraka kutoka kwa umma (wananchi)
na si chama cha siasa. Hakuna chama ambacho kiko madarakani isipokuwa kuna
serikali ya wananchi iliyoko madarakani. Rais aliyepo ni wa umma si wa chama
cha siasa – hakupata madarakani kutokana na chama siasa bali umma uliomchagua
kutoka kwa watu wenye vyama na hata wasio na vyama.
Tumeona
hata bunge linaendeshwa kiubaguzi wakati ni taasisi ya umma ambayo kamwe
haipaswi kujinasibisha na vyama vya siasa kwa kuwa hata wabunge/wawakilishi
wanatokana na wananchi na si chama cha siasa. Kazi inayofanywa na vyama vya
siasa ni kuendesha mchakato tu wa kupata wagombea ambao mwishowe huchaguliwa na
wananchi wote kuwa madiwani au wabunge. Tunashuhudia uhasama miongoni mwa
wananchi unaotokana na kuegemea chama fulani na kuleta mgawanyiko unaohatarisha
au kuvunja kabisa umoja wetu wa kitaifa. Lazima tuwe na masuala tunayokubaliana
kitaifa na kuyapa kipaumbele.
Ni
aibu kuona wanasiasa wakiunganishwa na misiba tu badala ya ajenda na masuala ya
kitaifa. Mbaya zaidi ni pale ambapo mbunge akifukuzwa au akikiacha chama chake
ananyang’anywa ubunge ambao alipewa na wananchi waliomchagua. Wananchi
wananyang’anywa demokrasia yao na mbunge wao. Hii ni dhambi kubwa! Chaguo la
wananchi halina budi kulindwa kikatiba na wananchi ndio wanaopaswa kumweka mtu
madarakani au kumwondoa. Ipo haja ya kuweka na kuulinda msimamo huu kikatiba.
Aidha,
chama chochote cha siasa kinachotaka kujijenga kwenye mioyo ya wananchi hakina
budi kuacha kujijenga chenyewe bali kishiriki kulijenga taifa na kushughulikia
matatizo yanayowakabili wananchi. Si busara kununua gari la kuendeshea kampeni
za kisiasa huku zahanati, kituo cha afya au hospitali ikiwa haina gari ya wagonjwa
au kuhudumia wajawazito. Chama cha siasa kikiamua kuchimba kisima, kuchonga
madawati au kujenga madarasa badala ya kujenga ofisi ya chama kinakuwa
kimejiwekea msingi mzuri miongani mwa jamii. Sioni mantiki ya kutumia mabilioni
ya pesa kufanya kampeni za kumpata mbunge huku tukishindwa hata kujenga
zahanati katika kijiji kimoja. Wala hatuna haja ya kuwa kadi za vyama vya siasa
kwa kuwa chama kinapaswa kugusa na kuishawishi mioyo ya watu na matatizo yao
hatimaye ndipo hupendwa na kuungwa mkono, na pengine kwa dhati zaidi kuliko
wenye kadi. Na kwa kipengele hiki napendekeza Chama Cha Mapinduzi kibadili
malengo yake pamoja na jina. CHADEMA kiache kuiga mwenendo wa CCM, na iwe vivyo
hivyo kwa vyama vingine.
4. Suala la
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar
Awali
ya yote, kama alivyowahi kusema Mwalimu Nyerere kuwa ukimwambia mtu mzima
ukweli unamheshimu, lakini ukimwambia uongo unamdharau. Ni kuwadharau wananchi
kuendelea kuwaambia kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ina serikali mbili.
Kusema ukweli tuna serikali za aina nne
hapa nchini – na si mbili kama ambavyo wengi wameaminishwa. Serikali hizo ni:
- Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar (SMZ) ambayo imekuwa wazi sana kiutendaji na kimuundo
- Serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SJMT/URT) ambayo ilianza na masuala 11
wakati wa kuanza muungano mnamo Aprili 26, 1964
- Serikali ya
Tanganyika ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikijificha kwenye masuala ya
muungano au kama ambavyo wengine kimakosa wamebuni jina la Tanzania Bara
- Serikali za
mitaa ambazo zinatenda kazi katika ngazi ya vitongozi, mitaa, vijiji,
wilaya, miji, manispaa na majiji.
Na
ieleweke kuwa Tanganyika na Zanzibar hazikufuta hadhi ya kuwa nchi isipokuwa tu
katika masuala ambayo ni ya muungano, na kwa miezi kadhaa baada ya kuungana, nchi
ya muungano iliendelea kuitwa Jamhuri ya
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar hadi pale ambapo mshindi wa kutunga jina
moja la muungano alipounganisha TAN kutoka
kwenye herufi tatu za kwanza za Tanganyika
na ZAN kutoka kwenye herufi tatu za
kwanza za Zanzibar, na kumalizia vifupisho
vya majina yake mawili vya I na A na kupata TANZANIA. Unapotaja TANZANIA
unataja mambo ambayo ni ya muungano, yanayobaki yanakuwa ya nchi ya Zanzibar upande mmoja wa muungano na
nchi ya Tanganyika kwa upande
mwingine.
Hadi
leo hakuna mahali popote ambapo jina Tanganyika lilifutwa na kuwekwa jina
lingine. Na hadi leo Hati ya Muungano
ndio mkataba pekee ulio hai kuhusiana na muungano wa nchi mbili. Wanaoita
Tanganyika kuwa ni Tanzania Bara wanakosea sana kwa kuwa hatujawahi kubadili
jina la Tanganyika kuwa Tanzania Bara. Hata tungekubaliana
kisheria bado tungekosea kuiita Tanganyika Tanzania Bara kwa kuwa pwani yote
(Mtwara, Lindi, Pwani, Dar es Salaam na Tanga) haiko bara! Aidha visiwa vya Mafia,
Songosongo, Koma, Kwale, Ukerewe na kwignineko haviko bara!
Nisisitize
kuwa, hali halisi na muundo halisi wa kiutendaji uliopo sasa tangu Aprili 26,
1964 ni wa serikali tatu: Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar, Serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali
ya Tanganyika ambayo kimakosa inajificha kwa kutumia jina la Tanzania au
Tanzania Bara. Pia kuna watu walijitungia kienyeji kwa kubdadili jina la Zanzibar
na kuita Tanzania Visiwani bila
kujua kuwa hata visiwa vya Ukerewe na Mafia ni Tanzania Visiwani lakini haviko
Zanzibar! Na waliendelea kutapatapa tena kwa kuiita Zanzibar Tanzania Zanzibar wakati ni Zanzibar na
ndiyo jina lililomo kwenye hati ya muungano. Nashukuru kwamba wazanzibar
wameendelea kuiita nchi yao kwa jina la Zanzibar.
Nisisitize
kuwa mambo yote yasiyo ya muungano yanashughulikiwa au yanasimamiwa na Zanzibar
au Tanganyika. Kusema masuala yasiyo ya muungano yanashughulikiwa na Tanzania
kwa upande wa Tangayika ni makosa kwa kuwa si ya muungano, maana Tanzania ni
kwa ajili ya masuala ya muungano tu! Wenzetu Zanzibar wanakwenda sawia na unavyosema
mkataba almaarufu Hati ya Muungano na wako wazi sana katika kufuata mkataba huo
na kuulinda.
Hadi
leo hii tuna sikukuu za aina tatu: uhuru wa
Tangnyika wa Desemba 9, mapinduzi ya
Zanzibar ya Januari 12 na muungano
wa Aprili 26. Kimahesabu huwezi kuunganisha vitu viwili ukabakiwa na vitu
viwili. Utakuwa na kimoja au zaidi ya viwili! Huwezi kuwaoza mwanamke na
mwanaume ukawa na ndoa mbili. Itakuwa ndoa moja tu. Ukiunganisha maumbo mawili
yaliyounganika kwa sehemu tu unapata maumbo matatu: kiunganiko (intersection
set) na sehemu mbili ambazo hazijaunganika. Kuendelea kusema uongo kwa kudai
kuwa Tanzania kuna serikali mbili wakati hali halisi kiutendaji ni serikali
tatu ni kuwadharau wananchi.
Tanganyika
ilikuwa na umri wa miaka miwili na miezi
mitano tu ilipoungana na Zanzibar kwa mambo 11 tu (sasa yako 22),
tangu ilipopata uhuru Desemba 9, 1961;
na Zanzibar ilikuwa na umri wa miezi
minne tu na siku kadhaa tangu ilipopata uhuru Desemba 10, 1963, na ilikuwa na umri wa miezi mitatu tu tangu ilipofanya mapinduzi Januari 12, 1964, ambayo ndiyo yanayoenziwa. Leo hii hatuwezi
kujigamba kwamba Zanzibar imefaidika na muungano kwa kuwa haikuishi muda mrefu
nje ya muungano (miezi mitatu tu) na kuzitumia vizuri fursa za kitaifa na
kimataifa. Na Tanganyika pia haikuishi muda mrefu nje ya muungano (miaka miwili
tu na miezi mitano). Tanganyika imekuwa ikigharamia mambo mengi ikiwa pamoja na
kuwaruhusu Wazanzibar washiriki bungeni kwa mambo yasiyo ya muungano wakati
Watanganyika hawashiriki kabisa kwa upande wa Zanzibar.
Nihitimishe
kwa kusema kuwa suluhisho muafaka na thabiti la kudumisha uhusiano mwema na
Wazanzibar ni kuwaachia kabisa wawe taifa huru na dola kamili kitaifa na
kimataifa. Tanganyika nayo ibakie kamili ili tuondokane kwa amani na kero
nyingi za muungano. Tubakie majirani wema kama ilivyo kwa Zambia, Msumbiji,
Rwanda, Kenya na kwingineko. Kuwa na mahusiano mema na jirani ni jambo la msingi
na si lazima muunganishe nchi. Kuna nchi nyingi tunahusiana nazo vizuri sana na
kwa ukaribu japo haziko jirani. Undugu ni mahusiano mema si kuunganisha nchi.
Zanzibar
imekosa fursa nyingi za kimataifa kwasababu ya kubanwa na kufinywa na muungano.
Kwao muungano ni jinamizi! Si vema kuendelea kuwabana watu ambao ni ndugu zetu
kama ilivyo kwa nchi zote jirani. Kuna faida nyingi kwa Tanganyika na Zanzibar
kuwa nje ya muungano. Hatuwezi kuendelea na serikali tatu na mifumo tata inayotugharimu
fedha nyingi na kero zisizoisha. Mungu ibariki Zanzibar, Mungu ibariki
Tanganyika, na bariki uhusiano wetu mzuri na wa kijadi kati ya Zanzibar na
Tanganyika na nchi zingine jirani na zilizo mbali.
No comments:
Post a Comment