Bi. AWILA- mwakilishi wa gazeti la mwananchi akiwa katika maandamano ya waandishi wa habari Tanzania kupinga mauaji ya mwandishi mwenzetu wa mkoani Iringa Marehemu Mwangosi. STANDARD RADIO FM 90.1 SINGIDA inalaani vitendo vya kikatili dhidi ya waandishi wa habari duniani kote. PICHA na. Prosper Kwigize
Na Evarista Lucas,
Singida
Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari
Singida(SINGPRESS) Bwana Seif Takaza; amewaasa wanahabari wa Mkoa wa Singida
kujipanga na kuwa wajasiri zaidi katika utekelezaji wa jukumu lao la uandishi
wa Habari.
Takaza alizungumza hayo mapema leo mara baada
ya kupokea maandamano ya wanahabari hao wa Mkoa wa Singida katika ofisi ya
SINGPRESS iliyopo katika jengo la CDTF mtaa wa Mughanga.
Waandishi wa Habari Mkoani Singida ambao
wameungana na waandishi wenzao nchini kwa maandamano ya kimya kimya kulaani na
kupinga vikali mauaji ya kikatili dhidi ya aliyekuwa mwandishi wa habari wa
kituo cha Channel Ten mkoani na Mwenyekiti w Klabu ya Waandishi wa Habari
Iringa marehemu Daudi Mwangosi, wakati akiwa kazini.
Maandamano hayo yakisindikizwa na askari polisi
yalianzia eneo la Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) na kupitia barabara ya
Kawawa hadi kituo cha mafuta Esso.
Baadaye yaliingia barabara ya Soko kuu,
msikitini, Mghandi, Ipembe, Karume, Kinyeto na hatimae kumalizikia kwenye ofisi
ya klabu, ambapo Mwenyekiti wa SINGPRESS, Seif Takaza aliyapokea.
Akizungumza na waandishi 19 wa mkoa Singida
walioshiriki maandamano hayo, Takaza alisema kitendo cha polisi kuhusika na
mauaji hayo kimedhalilisha chombo hicho, pia ni ukiukwaji wa haki za binadamu,
kulingana na mafunzo yao ya kijeshi.
“Mauaji ya mwangosi ni ya makusudi, hasa
ikizingatiwa alikuwa mikononi mwa polisi, lakini mwisho wa siku akafia mikononi
mwao….jambo hili lazima lipingwe kwa nguvu zote na watetezi wa haki za
binadamu,”alisema.
Alisema mauaji hayo ni ya uonevu, kikatili na
yanalifedhehesha taifa ambalo tangu lipate uhuru mwaka 1961 limejipatia sifa
kubwa ya kudumu katika hali ya amani na utulivu kiasi cha kuitwa jina la kisiwa
cha amani.
Aidha wanahabari hao wameomba kudumishwa kwa
mahusiano kati ya jeshi la polisi na waandishi wa habari ili kuondoa uwezekano
wa kutokea mauaji mengine kama hayo.
Hata hivyo wananchi wengi, waliyaunga mkono
maandamano hayo huku wakiwapungia mikono sanjari na ‘Poleni’, kila ambapo
wanahabari walipita katika barabara mbalimbali za mjini Singida.
Kwa upande upande mwingine baadhi ya
wanahabari waliopata fursa ya kutoa maoni yao na dukuduku dhidi ya mauaji hayo
ya kikatili walisema kuwa licha ya kuwa marehemu Mwangosi alikufa akiwa kazini;
ni wazi kuwa alitaka kuujulisha umma kile kinachoendelea na pia kujitaftia
riziki yake.
" Wamiliki waboreshe malipo ya Waandishi
wa habari haswa walioko mikoani kwakuwa kipato chao kinategemea zaidi utumaji
wa stori na inawezekana kuwa karehemu alipoteza maisha wakati akihangaika
kupata stori." Alisisitiza Josephat Isango ambaye anaandikia gazeti la
Tanzania Daima.
No comments:
Post a Comment