Na:Mwandishi wetu
Madiwani 16 wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA) wa halmashauri ya wilaya ya Hanang, mkoani Manyara juzi walisusia mkutano
wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo na kuamua kutoka nje ya ukumbi wakidai
kanuni za mkutano huo zimekiukwa.
Akizungumza na Waandishi wa habari nje ya ukumbi wa
mkutano huo, Mbunge wa viti maalum Mkoa wa Manyara kupitia tiketi ya CHADEMA, Bi.
Rose Kamili amesema madiwani hao
waligoma kujiandikisha kwenye orodha ya wajumbe baada ya kutokubaliana na
dondoo zilizokuwepo kwenye mkutano huo, ikiwemo ya uchaguzi wa makamu mwenyekiti
wa Halmashauri hiyo na kupitisha kamati za kudumu.
Aidha mbunge huyo amesisitiza pia kwamba licha ya
madiwani wa chama hicho kudai mabadiliko ya maamuzi hayo kabla ya kusoma
muhtasari wa kikao, mwenyekiti alitumia ubabe kulazimisha kikao hicho kuendela
na kwamba hakuwa tayari kusikiliza wazo la mtu ambaye hajajiandikisha kwenye
mahudhurio ya mkutano huo.
Akihalalisha kufanyika kwa mkutano huo, Mwanasheria wa TAMISEMI,Bw. Eustad
Atanas Ngatale amesisitiza kuwa taratibu za mikutano ya halmashauri zinaongozwa
na kanuni za uendeshaji wa mikutano ya halmashauri ambazo zinatungwa na halmashauri
yenyewe lakini uwezo huo umetolewa na Waziri mwenye dhamana ya serikali za mitaa.
No comments:
Post a Comment