Na:Mwandishi wetu
Wilaya ya Simanjiro iliyoko mkoani Manyara, inaongoza kwa kufikiwa
na kukaliwa na wahamiaji haramu ikilinganishwa na wilaya nyiingine za mkoa huo.
Katibu Tarafa wa Moipo, Bw. Joseph Mtataiko, amesema hayo wakati
akifungua warsha iliyoandaliwa na Idara ya Uhamiaji Mkoa, kuhusu ulinzi
shirikishi kwa kuwatambua na kuwafichua wahamiaji haramu.
Amesema wilaya hiyo ni maficho ya wahamiaji haramu kutokana
na mgodi wa machimbo ya madini wa Mererani, kwani kila siku wageni wapya
wanaingia kutoka sehemu mbalimbali nchini hasa mikoani.
Aidha, amesema wilaya hiyo ni mapito ya wageni haramu waendao
nchi za jirani za kusini mwa Tanzania. Kamishna Msaidizi wa Uhamiaji mkoani
Manyara, Ebros Mwanguku, amewataka wananchi wa wilaya hiyo kuwa makini kwa
wageni wanaoingia kwa kutoa taarifa katika kituo cha polisi, ili wafanyiwe
uchunguzi kuhusu uingiaji wao wilayani humo.
Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Manyara imeendesha warsha ya
uhamiaji shirikishi ikishirikisha kamati za ulinzi na usalama, katika wilaya za
Babati, Mbulu na Simanjiro na kumalizia na wilaya za Kiteto na Hanang’ ili
kuimarisha ulinzi na hali ya usalama na amani mkoani humo.