Sunday, December 9, 2012

TAMKO LA WAANDISHI WA HABARI DAR ES SALAAM

Kufuatia kupigwa risasi, kujeruhiwa begani na kulazwa katika
hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa mwandishi wa Tanzania Daima Bwana
Shabani Matutu (30) ambaye pia ni mwanachama hai wa Dar City Press
Club(DCPC), uongozi wa Klabu uliamua kufuatilia tukio hilo kwa karibu
ili kujua na kuhakiki kwa kina yaliyotokea na sababu zilizopelekea
hayo kutokea.

Kutokana na hayo DCPC imebaini yafuatayo.
1. Ni kweli kwamba Shabaan matutu(30) alipigwa risasi na askari
wa jeshi la Polisi mwenye namba F.8991 D/C Idrissa nyumbani kwa
Shabaan kimakosa baada ya askari huyo na wenzake wanne kufungua kwa
nguvu na bila ya kujitambulisha kwa mwenye nyumba (Shabaan na Mkewe)
licha ya kuombwa kufanya hivyo kabla.

2. Kuna maelezo yanayokinzana katika kuelezea jinsi tukio hilo
lilivyotokea kwa pande mbili zinazohusika yaani maelezo ya shabaan na
ya polisi

3. Kwamba sababu za askari polisi hao kufanya hivyo hazikuwa
zimefanyiwa uchunguzi wa kutosha hadi kujiridhisha kuchukua hatua hiyo
hivyo hata wao walikiri kukosea pamoja na kueleza kwamba Shabaan ndiye
aliyeaanza kuwashambulia askari Polisi kabla ya wao kumjeruhi kwa
risasi.

4. Shabaan mpaka sasa anaendelea na matibabu licha ya kuuguza
majeraha aliyosababishiwa na polisi na kwamba ameshauriwa kitaalamu
kupumzika nay eye binafsi ameomba asibughudhiwe ili afya yake irejee
haraka na kwamba pindi atakapokuwa katika hali nzuri zaidi ya sasa kwa
mujibu wa ushauri huo wa kitabibu, atawasiliana na yeyote wakiwemo
polisi ambao wamekuwa wakimmghasi kwa kuja kumhoji mara kwa mara.

Kwa sababu hizo basi Dar es salaam City Press Club

1. Tunaiomba Serikali na mamlaka za juu zaidi ya jeshi la Polisi
hususan Wizara ya mambo ya ndani ifanye uchunguzi wa kina na huru
wenye kuhusisha taasisi wakilishi katika jamii juu ya tukio hilo na
kulichunguza jeshi la polisi linavyofanya kazi zake kwa kuzingatia
kanuni na sheria.
2. Tunalitaka Jeshi la Polisi liache mara moja kutuma askari wake
kwenda kwa Shabaan kwa lengo la kumhoji ama kutaka atoe maelezo yake
kwa viongozi wa jeshi hilo ilhari walishamtuhumu na kueleza kuwa
aliwashambulia Polisi kwa Panga kabla ya wao kumfyatulia risasi.
Tunasema hivi kwa kuzingatia kanuni za afya na haki za msingi za
binadamu.
3. Tunalitaka Jeshi la Polisi liueleze umma bila kuficha ukweli
na kwa jinsi ile ile ambayo lilitoa taarifa mara baada ya tukio,
lieleze kwa nini linatumia habari na vyanzo dhanifu kujeruhi na
kuhatarisha maisha ya raia wasio na kosa huku likitoa maelezo
yasiyofanyiwa uchunguzi.
4. Mwisho tunalitaka jeshi la Polisi lenyewe lijitafiti na
kujipanga upya ili liweze kufanya kazi kisayansi na weledi kama
ambavyo viongozi wake wamekuwa wakijinadi mbele ya vyombo vya habari.
Tamko hili limetolewa leo Tarehe 08/Desemba/2012.

Joseph Kayinga
Katibu Mkuu-DCPC

No comments: