Thursday, April 25, 2013

VIJANA WAPEWA SOMO-MATUMIZI YA VIDHIBITI MIMBA


Source: SR/Monica

Ed: BM

Date: 25 April 2013.

 SINGIDA

Vijana wametakiwa kutojihusisha na matumizi ya vidhibiti mimba pasipo kujua madhara yake.

Hayo yamesemwa na Bi Judith Kattani mratibu wa Pro-life Tanzania jimbo la Singida na Kahama, alipokuwa akizungumza katika kipindi cha Hoja ya leo jana kinachotangazwa na Standard Radio.

Amesema kuwa vijana wengi wanaathirika na madawa hayo pasipo kujua kutokana na kukosa elimu ya kutosha.

 Bi Judith amesema kutokana na matumizi hayo ya vidhibiti mimba yanachangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la maambukizi ya virusi vya ukimwi kwa vijana kutokana na kuendekeza mapenzi na kujisahau katika utekelezaji wa majukumu yao.

 Mratibu huyo wa Pro-life Tanzania Bi Judith Kattani ametoa wito pia kwa wanafunzi kutojihusisha na vitendo vya mapenzi wakati wa masomo, jambo ambalo linachangia kwa kiasi kikubwa kushuka kwa kiwango cha elimu kutokana na matumizi hayo ya vidhibiti mimba yanayowafanya kujiamini kuwa hawawezi kupata mimba, jambo ambalo ni hatari kwao kwani huzuia mimba na kusahau kuwa kuna gonjwa la ukimwi.

 Aidha Bi Judith amewaasa wazazi kutoa ushirikiano kwa walimu ili kushirikiana kwa pamoja kuweza kuwalea watoto ili kukuza maadili ya vijana, kwani bila kufanya hivyo kiwango cha elimu kitazidi kushuka na maambukizi ya virisi vya ukimwi yatazidi kuongezeka.

CHANJO KWA WATOTO MKOANI SINGIDA

Na. Elisante John, Singida
 
WATOTO 997 Mkoani Singida wenye umri wa chini ya mwaka mmoja, wanatarajia kupata chanjo wakati wa wiki ya chanjo kitaifa, inayoendelea kufanyika nchini kote.

Hayo yamebainishwa na Mganga mkuu Mkoa wa Singida, Dk.Dorothy Kijugu na kubainisha kuwa jumla ya vituo 178 vitatumika kwa ajili ya kufanikisha zoezi hilo, lililoanza juzi Aprili 22 hadi 28, mwaka huu.



Naye mgeni rasmi katika uzinduzi huo uliofanyika leo kwenye kituo cha afya Sokoine Mjini Singida, Mwalimu Queen Mlozi amesifu jitihada zinazofanywa na wauguzi hadi kufikia mkoa kushika nafasi ya kwanza mwaka jana juu ya zoezi hilo na akawataka mwaka huu ushike nafasi ya kwanza.
Katika uzinduzi huo, Dk. Kijugu amesema kwa mujibu wa takwimu za shirika la afya Duniani (WHO) chanjo hizo kwa watoto chini ya mwaka mmoja zinazuia vifo takribani milioni mbili hadi tatu kila mwaka.

Thursday, March 28, 2013

TAARIFA YA HABARI KUTOKA STANDARD RADIO


Source; SR/ Neema J

Ed;

Date; March, 27, 2013

 

SINGIDA

Mkuu wa wilaya ya singida  Bi Queen Mlozi,  amelita jeshi la polisi  kutumia mafunzo watayoyapata  ipasavyo,  na kusema yatawasaidia kuongeza maarifa mapya  na kuleta  mabadiliko,  kwa kuwajibika  katika utendaji kazi wao.

Akizungumza katika uzinduzi wa mafunzo ya jeshi polisi kazini jana Bi Mlozi amesema, maendeleo hayawezi kuja bila changamoto, hivyo  kuwataka polisi  kuhamasishana  katika utendaji kazi wao,   bila kukata tamaa kwani elimu haina mwisho.

Kwa upande wake kamanda wa polisi mkoa wa Singida ACP Linus Sinzumwa, amesema lengo la mafunzo hayo  kutawezesha  afisa  askari  na polisi  ufanisi wa kufanya kazi,  kuleta mabadiliko katika utendaji  kazi wao,  pamoja na kuliwezesha jeshi la polisi kufanya kazi kwa  ufanisi, usasa,  uweledi  pamoja kushirikishaisha jamii, juu ya ulinzi  wa mali zao.

Naye mkufunzi wa   elimu ya watu wazima mkoa wa singida Bw Musa Nkungu,  ambaye ni mmoja  kati ya  watoa mafunzo  kwa jeshi la polisi,  amesema  mafunzo hayo yatawasaidia polisi kupata mafaniko,  ikiwa ni pamoja na  muhitimu   kutunikiwa cheti atakapo hitimu  mafunzo kazini,  na kupandishwa cheo  na kuongezewa madaraka  ya uongozi, katika jeshi la polisi  hivyo kuwataka polisi kuhudhuria katika mafunzo, ili waongeze ufanisi wa kazi .

 

Source; Tanzania Daima

Ed;

Date; March, 27, 2013

DAR ES SALAAM

Serikali imesema haitamvumilia mtu atakayeendesha shughuli za kibinadamu, katika maeneo tengefu  lengo ni kunusuru ikolojia ya Hifadhi za Serengeti, Ngorongoro na Loliondo.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, amesema wananchi walioingia ndani ya pori tengefu la Loliondo, wanatakiwa kuondoka mara moja.

Balozi Khagasheki amesema kutokana na mgogoro ulioko Loliondo kwa muda mrefu sasa, serikali imepata ufumbuzi ambapo wananchi wanatakiwa kutii sheria bila kushurutishwa.

Aidha amesema ili, kutatua migogoro iliyopo serikali itatenga na kuchukua sehemu ya ardhi ya Pori Tengefu la Loliondo, yenye ukubwa wa kilomita za mraba 1500 kutoka kwenye eneo la kilomita za mraba 4000, za pori hilo.

Source; SR/ Elizabeth, Martine

Ed;

Date; March, 27, 2013

 

SINGIDA

Wanachama wa chama cha walemavu wasiioona mkoani Singida TLB, wanakabiliwa na changamoto mbalimbali katika maisha yao ya kila siku, na kusababisha kushindwa kutekekeleza majukumu yao.

Akizungumza na standard radio mwenyekiti wa chama cha walemavu wa kutoona mkoani singida Bw. Hassani kingugu , ambaye pia ni mlemavu wa kutoona amesema kuwa, changamoto zimekuwa ni tatizo katika maisha yao jambo linalopelekea wao kushindwa kumudu maisha, na kubaki wanahangaika.

Bw. Kingugu amezitaja changamoto hizo kuwa  ni jamii kuwa na mtazamo hasi kwa kudhani walemavu hawawezi kitu, uhaba wa shule, vifaa vya kujifunzia na kufundishia, kubadilika kwa mitaala, kutoshirikishwa kwenye shughuli za ujasiriamali, pamoja na viongozi mbalimbali kutowaelimisha wanajamii, namna ya kuwajali na kuwahudumia walemavu wasioona.

Aidha ametoa wito kwa jamii kutowabagua walemavu na badala yake itambue mchango wao katika maisha ya kila siku, kwani kuna walimu ,wafanyabiashara, mahakimu ambao ni walemavu.

Source; Tanzania Daima

Ed;

Date; March, 27, 2013

TANGA

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Luteni mstaafu Chiku Galawa, amesema tatizo la vijana wengi kukosa ajira linaweza kumalizika ikiwa watavitumia vyuo vya ufundi stadi (VETA), vilivyopo katika maeneo yao.

Mkuu huyo wa mkoa ametoa kauli hiyo katika ziara yake ya kutembelea chuo cha Veta cha jijini Tanga, kwa lengo la kujua hatma ya vijana hao, kupatiwa nafasi mbalimbali, ili hatimaye waondokane na tabia ya kurandaranda mitaani.

Galawa ametumia fursa hiyo kuwataka vijana kutambua fursa hiyo, akiwahakikishia kwamba wanaweza kujikwamua na suala la umaskini, linalowakabili vijana wengi, kutokana na kukosa shughuli za kufanya.
Naye Mkurugenzi wa Chuo cha Ufundi Veta Tanga, Alphonce Kibasha, amemwambia mkuu wa mkoa kwamba changamoto inayowakabili ni uhaba wa majengo, ya kuweza kuchukua vijana wengi kwa wakati mmoja.

Monday, March 25, 2013

HABARI KUTOKA STANDARD RADIO FM 90.1 MHz

Source:SR/E. Lyatuu.

Ed: BM

Date: March 25, 2013.

 

SINGIDA

Jamii katika manispaa ya Singida, imetakiwa kutoona vijana ni mzigo badala yake ione kuwa vijana ni suluhisho la kuleta mabadiliko ya kimaendeleo katika nchi, ili kuondokana na umaskini kwa kuwa vijana ni nguzo ya taifa.

 

Bw. Fidelis Yunde Mratibu na mwanzilishi wa shirika la harakati za vijana katika kuleta maendeleo, Youth Movement for Change YMC amesema hayo, wakati akizungumza na standard radio ofisini kwake, kuhusiana na fursa za vijana katika jamii, mapema leo.

 

Bw. Yunde amesema jamii inapaswa kuwapa vijana hamasa kwa kuwahamasisha, kuwapa nafasi mbali mbali za uongozi kwa kuamini wanaweza, kama vile uongozi katika siasa, kwani wao ni mabalozi wazuri katika vita dhidi ya umaskini.

 

Aidha, amewataka vijana kuunda vikundi mbali mbali kama vile vya kiutamaduni, ujasiriamali, ili kujua jinsi ya kubuni, kuanzisha na kuboresha biashara kwa kupata elimu kuhusu maendeleo ya vijana, na kuchukua hatua kubadili vijiwe vyao kuwa vijiwe vya kazi ili kuleta maendeleo. Amesema vijana wajitume kwa kujishughulisha katika fursa zilizopo kama vile kilimo kwanza, pia viongozi wawekeze zaidi kwa vijana kwa kutoa nafasi za uongozi.

 


Source:Tanzania Daima

Ed: BM

Date: March 25, 2013.

DAR ES SALAAM

Meneja wa wafanyakazi wa ndani ya ndege wa Kampuni ya FastJet, Emma Donavan anayedaiwa kutoa lugha ya matusi kwa mfanyakazi mwenzake, leo amefikishwa mahakamani.

Donavan amefikishwa mahakamani baada ya polisi kukamilisha kazi ya kumhoji sambamba na mashahidi wengine na kisha jalada lake kufikishwa kwa Mkurugenzi wa Mashitaka nchini DPP, ambaye naye baada kumaliza kulipitia alilirudisha polisi, ili taratibu za kwenda mahakamani ziendelee.

Meneja huyo anakabiliwa na tuhuma za kutoa lugha ya matusi kwa mfanyakazi mwenzake, Samson Itembe. Wiki iliyopita, Kamanda wa Polisi wa Viwanja vya Ndege, Deusdedit Kato, alisema walimaliza kumhoji Emma na jalada kupelekwa kwa DPP.

Habari kutoka Kituo cha Polisi cha Mamlaka ya Viwanja vya Ndege katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu JK Nyerere -Terminal One -  zinasema polisi wamekuwa wakikukusanya ushahidi kutoka kwa wafanyakazi wengine kabla ya jalada kupelekwa kwa DPP.

Meneja huyo ambaye ni raia wa Uingereza alikamatwa wiki iliyopita baada ya kusakwa kwa siku kadhaa.

Source:SR/Bandola.

Ed: BM

Date: March 25, 2013.

 

SINGIDA

Chama Cha Mapinduzi CCM kimewaomba wamiliki halali wa eneo la Nkonkilangi Shelui  katika wilaya ya Iramba mkoani Singida, kuwaruhusu wachimbaji wadogo wadogo wasio na leseni kuendelea kuchimba ili kujipatia riziki.

 

Kauli hiyo imetolewa leo na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi mkoa wa Singida Bw. Mgana Msindai wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za chama hicho mkoani humu.

 

Bw. Msindai amesema kuwa wachimbaji wadogo wadogo wasio na leseni ndiyo walioomba CCM  Mkoa iwasaidie waruhusiwe kuendelea kuchimba na kwenye kikao cha kamati ya siasa mkoa, kilikubaliana chama kisaidie kuwaokoa wananchi wa Nkonkilangi waendelee kujipata riziki zao.

Aidha Bw. Msindai amesema hayo kufuatia mwandishi wa gazeti la Tanzania Daima  Shehe Semtana aliyeandika kuwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi CCM mkoani Singida, Bw. Mgana Msindai anatuhumiwa  kupora machimbo ya madini ya wachimbaji wadogo wadogo katika kijiji cha Nkonkilangi na kumkabidhi Bw John Bina bila ridhaa ya wanakijiji.

 

 

Source:SR/Saada

Ed: BM

Date: March 25, 2013.

SINGIDA

Kamishna msaidizi wa madini kanda ya Kati Bw. Manase Mbasha, amewataka wachimbaji wadogo wadogo wa madini kukata leseni, kulingana na maeneo waliyo na uwezo nayo, na kuacha kutegemea wafadhili na wawekezaji.

Bw. Mbasha amesema hayo leo, wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kutokana na umhimu wa wachimbaji kukata leseni kulingana na maeneo waliyo na uwezo nayo, na kuacha kuomba leseni ya kumiliki maeneo makubwa ambayo hawana uwezo wa kuyafanyia kazi.

Aidha, Bw. Mbasha ametaja maeneo yenye wachimbaji wadogo wadogo mkoani Singida kuwa ni, Misigiri, Mpambaa, Msangachuki, Londoni, Sekenke, na Nkonkilangi.

Amesema ofisi yake inakaribia kutoa leseni kwa wachimbaji wa madini ya shaba, chumvi, zilikoni, na madini ya chuma.


Source:SR/Saada

Ed: BM

Date: March 25, 2013.

 

DAR ES SALAAM

Rais wa China Xi Jinping leo amehutubia dunia kutokea nchini Tanzania kuelezea sera ya serikali ya China kwa Bara la Afrika.

Hotuba hiyo imetolewa mara baada ya kuzindua na kukabidhi rasmi kituo cha mikutano cha kimataifa cha Mwalimu Julius Nyerere, jijini Dar es salaam kilichojengwa kwa msaada wa serikali ya China kwa lengo la kumuenzi Mwalimu Nyerere.

Rais huyo wa China amesaini mikataba kumi na saba na rais Jakaya Kikwete, na baadaye ametembelea makaburi ya wataalam wa kichina yaliyopo katika kijiji cha Majohe-Ukonga, ambapo ametoa heshima zake kwa wachina waliofariki wakati wakijenga reli ya TAZARA.

Rais Xi Jinping ameondoka nchini leo jioni kuelekea nchini Afrika kusini kuhudhuria mkutano wa tano wa wakuu wa nchi za BRICS ambazo ni Brazil, India, China na Afrika kusini.