Ed: BM
Date: March 25, 2013.
SINGIDA
Jamii katika manispaa ya Singida,
imetakiwa kutoona vijana ni mzigo badala yake ione kuwa vijana ni suluhisho la
kuleta mabadiliko ya kimaendeleo katika nchi, ili kuondokana na umaskini kwa
kuwa vijana ni nguzo ya taifa.
Bw. Fidelis Yunde Mratibu na
mwanzilishi wa shirika la harakati za vijana katika kuleta maendeleo, Youth
Movement for Change YMC amesema hayo, wakati akizungumza na standard radio
ofisini kwake, kuhusiana na fursa za vijana katika jamii, mapema leo.
Bw. Yunde amesema jamii inapaswa
kuwapa vijana hamasa kwa kuwahamasisha, kuwapa nafasi mbali mbali za uongozi
kwa kuamini wanaweza, kama vile uongozi katika siasa, kwani wao ni mabalozi
wazuri katika vita dhidi ya umaskini.
Aidha, amewataka vijana kuunda
vikundi mbali mbali kama vile vya kiutamaduni, ujasiriamali, ili kujua jinsi ya
kubuni, kuanzisha na kuboresha biashara kwa kupata elimu kuhusu maendeleo ya
vijana, na kuchukua hatua kubadili vijiwe vyao kuwa vijiwe vya kazi ili kuleta
maendeleo. Amesema vijana wajitume kwa kujishughulisha katika fursa zilizopo
kama vile kilimo kwanza, pia viongozi wawekeze zaidi kwa vijana kwa kutoa
nafasi za uongozi.
Source:Tanzania Daima
Ed: BM
Date: March 25, 2013.
DAR ES SALAAM
Meneja wa wafanyakazi wa ndani ya ndege wa
Kampuni ya FastJet, Emma Donavan anayedaiwa kutoa lugha ya matusi kwa
mfanyakazi mwenzake, leo amefikishwa mahakamani.
Donavan amefikishwa mahakamani baada ya polisi
kukamilisha kazi ya kumhoji sambamba na mashahidi wengine na kisha jalada lake
kufikishwa kwa Mkurugenzi wa Mashitaka nchini DPP, ambaye naye baada kumaliza
kulipitia alilirudisha polisi, ili taratibu za kwenda mahakamani ziendelee.
Meneja huyo anakabiliwa na tuhuma za kutoa
lugha ya matusi kwa mfanyakazi mwenzake, Samson Itembe. Wiki iliyopita, Kamanda
wa Polisi wa Viwanja vya Ndege, Deusdedit Kato, alisema walimaliza kumhoji Emma
na jalada kupelekwa kwa DPP.
Habari kutoka Kituo cha Polisi cha Mamlaka ya
Viwanja vya Ndege katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu JK Nyerere
-Terminal One - zinasema polisi wamekuwa
wakikukusanya ushahidi kutoka kwa wafanyakazi wengine kabla ya jalada kupelekwa
kwa DPP.
Meneja huyo ambaye ni raia wa Uingereza
alikamatwa wiki iliyopita baada ya kusakwa kwa siku kadhaa.
Source:SR/Bandola.
Ed: BM
Date: March 25, 2013.
SINGIDA
Chama Cha Mapinduzi CCM kimewaomba wamiliki
halali wa eneo la Nkonkilangi Shelui
katika wilaya ya Iramba mkoani Singida, kuwaruhusu wachimbaji wadogo
wadogo wasio na leseni kuendelea kuchimba ili kujipatia riziki.
Kauli hiyo imetolewa leo na Mwenyekiti
wa Chama Cha Mapinduzi mkoa wa Singida Bw. Mgana Msindai wakati akizungumza na waandishi
wa habari katika ofisi za chama hicho mkoani humu.
Bw. Msindai amesema kuwa wachimbaji
wadogo wadogo wasio na leseni ndiyo walioomba CCM Mkoa iwasaidie waruhusiwe kuendelea kuchimba
na kwenye kikao cha kamati ya siasa mkoa, kilikubaliana chama kisaidie kuwaokoa
wananchi wa Nkonkilangi waendelee kujipata riziki zao.
Aidha Bw. Msindai amesema hayo
kufuatia mwandishi wa gazeti la Tanzania Daima
Shehe Semtana aliyeandika kuwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi CCM mkoani
Singida, Bw. Mgana Msindai anatuhumiwa kupora machimbo ya madini ya wachimbaji wadogo
wadogo katika kijiji cha Nkonkilangi na kumkabidhi Bw John Bina bila ridhaa ya
wanakijiji.
Source:SR/Saada
Ed: BM
Date: March 25, 2013.
SINGIDA
Kamishna msaidizi wa madini kanda ya Kati Bw.
Manase Mbasha, amewataka wachimbaji wadogo wadogo wa madini kukata leseni,
kulingana na maeneo waliyo na uwezo nayo, na kuacha kutegemea wafadhili na
wawekezaji.
Bw. Mbasha amesema hayo leo, wakati akizungumza
na waandishi wa habari ofisini kwake kutokana na umhimu wa wachimbaji kukata
leseni kulingana na maeneo waliyo na uwezo nayo, na kuacha kuomba leseni ya
kumiliki maeneo makubwa ambayo hawana uwezo wa kuyafanyia kazi.
Aidha, Bw. Mbasha ametaja maeneo yenye
wachimbaji wadogo wadogo mkoani Singida kuwa ni, Misigiri, Mpambaa,
Msangachuki, Londoni, Sekenke, na Nkonkilangi.
Amesema ofisi yake inakaribia kutoa leseni kwa
wachimbaji wa madini ya shaba, chumvi, zilikoni, na madini ya chuma.
Source:SR/Saada
Ed: BM
Date: March 25, 2013.
DAR ES SALAAM
Rais wa China Xi Jinping leo amehutubia dunia
kutokea nchini Tanzania kuelezea sera ya serikali ya China kwa Bara la Afrika.
Hotuba hiyo imetolewa mara baada ya kuzindua na
kukabidhi rasmi kituo cha mikutano cha kimataifa cha Mwalimu Julius Nyerere, jijini
Dar es salaam kilichojengwa kwa msaada wa serikali ya China kwa lengo la
kumuenzi Mwalimu Nyerere.
Rais huyo wa China amesaini mikataba kumi na
saba na rais Jakaya Kikwete, na baadaye ametembelea makaburi ya wataalam wa
kichina yaliyopo katika kijiji cha Majohe-Ukonga, ambapo ametoa heshima zake
kwa wachina waliofariki wakati wakijenga reli ya TAZARA.
Rais Xi Jinping ameondoka nchini leo jioni
kuelekea nchini Afrika kusini kuhudhuria mkutano wa tano wa wakuu wa nchi za
BRICS ambazo ni Brazil, India, China na Afrika kusini.
No comments:
Post a Comment