Na. Boniface Mpagape
Serikali kupitia wizara ya maliasili na
Utalii imeanzisha siku ya utundikaji mizinga kitaifa mwaka huu, kwa lengo la
kuongeza msukumo katika sekta hiyo yenye uwezo wa kuondoa umaskini.
Taarifa iliyotolewa na Mkuu wa mkoa wa
Singida Dk. Parseko Kone kwa vyombo vya habari leo, imesema uzinduzi wa mkakati
huo kitaifa utafanyika Machi 4, wilayani Manyoni mkoani Singida na Waziri mkuu
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Bw. Mizengo Peter Pinda anatarajiwa kuwa
mgeni rasmi.
Dk. Kone amesema hii ni heshima kubwa
kwa mkoa wa Singida na wananchi wake na ni heshima kwa wafuga nyuki wote wa
mkoa wa Singida.
Amesema ufugaji nyuki ni njia sahihi ya
kutumia raslimali za misitu katika kujiongezea kipato, badala ya kuharibu
mazingira kwa kukata miti ili kuchoma mkaa kwani ufugaji huo unatunza miti kwa
sababu ni chanzo kikuu cha asali.
Amewataka wananchi wa mkoa wa Singida
kutumia fursa hiyo kwa kuongeza idadi ya mizinga katika mashamba yao, na wale
ambao hawajaanza waanze leo. Mkuu wa mkoa wa Singida ametoa ushauri kujiwekea
lengo la kutundika mizinga angalau mitano kila mwaka.
Aidha, amewaomba wananchi wote siku ya
tarehe 4 Machi mwaka huu, kujitokeza kwa wingi katika hifadhi ya nyuki ya
Aghondi wilayani Manyoni, ili kushuhudia uzinduzi na kujifunza mbinu mbali
mbali za kisasa za ufugaji nyuki.
Kauli mbiu ya siku ya taifa ya
utundikaji mizinga mwaka huu, ni Fuga nyuki uongeze kipato, tundika mizinga.
No comments:
Post a Comment