Na. Boniface Mpagape.
Mkoa wa Singida
umeazimia kuweka kipaumbele kwa mazao yanayostahimili ukame ambayo ni mtama,
uwele na viazi vitamu ili kuondokana na tatizo la upungufu wa chakula.
Maazimio hayo
yamefikiwa katika kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa kilichofanyika katika
ukumbi wa mikutano wa VETA mkoni humo. Mwenyekiti wa kikao hicho, mkuu wa mkoa
wa Singida Dk. Parseko Ole Kone amesisitiza wakulima kulima mazao
yanayostahimili ukame, ili kwenda sambamba na hali ya hewa mkoani Singida,
kutokana na ukame unaoukabili mkoa huo.
Akizungumza katika
ufunguzi wa kikao hicho Dk. Kone amesema kwa zaidi ya miaka mitatu mkoa umekuwa
na ongezeko la uzalishaji wa mazao ya chakula kutoka tani 442,180 mwaka 2009/2010
hadi tani 575,228 mwaka 2012, sawa na ongezeko la asilimia 30.
Amesema uzalishaji wa
mazao ya biashara umeongezeka kutoka tani 164,673 mwaka 2009/2010 hadi tani
289,305 mwaka 2011/12 sawa na ongezeko la asilimia 76, na kwamba mafanikio hayo
yanatokana na Mkoa kuteua na kufanya juhudi ya kuendeleza mazao ya kipaumbele
kwa kuzingatia hali ya hewa. Ameyataja mazao yaliyochaguliwa kwa ajili ya
chakula ni mtama, uwele, viazi vitamu na mikunde na mazao ya biashara ni
alizeti, pamba, vitunguu na asali.
Wajumbe wa kikao hicho
kwa kauli moja, wameazimia kuweka msisitizo wa kuzalisha mazao hayo na kwamba
uhamasishaji ufanyike ili wakulima washiriki kikamilifu katika kuzalisha mazao
hayo.
Aidha, wajumbe wa kikao
hicho wamependekeza sheria ndogo ndogo
zitungwe katika kila halmashauri mkoani Singida, ili kuhakikisha kila
kaya inakuwa na hekari walau tatu za mazao yanayostahimili ukame, ambayo ndiyo
mkobozi kwa wakulima kuondokana na tatizo la uhaba wa chakula. Suala la
matumizi mabaya ya chakula pia limejadiliwa katika kikao hicho na wakulima
wametakiwa kutumia vizuri chakula wanachokipata.
Wajumbe wa kikao hicho
pia wamejadili taarifa ya maendeleo ya elimu mkoani Singida, ambapo imeelezwa
kuwa matokeo ya kidato cha nne mwaka 2012 mkoa wa Singida ni mabaya. Afisa
elimu wa mkoa wa Singida Bi. Fatuma Kilimia amesema mkoa umeweza kufaulisha
daraja la kwanza hadi la nne wanafunzi 2272, sawa na asilimia 23.8 kati ya
wanafunzi 9,536 waliofanya mitihani hiyo.
Kutokana na takwimu
hizo, amesema wanafunzi 7264 sawa na asilimia 76.2 walifeli kwa kupata daraja
sifuri.
No comments:
Post a Comment