Wednesday, November 6, 2013

EAC YATARAJIA KUANZA MAZUNGUMZO RASMI NA SUDAN KUSINI








Na.Mwandishi wetu
Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), inatarajia kuanza mazungumzo na Serikali ya Sudan Kusini yatakayohusisha timu ya ngazi ya juu ya wajumbe watatu kutoka nchi wanachama kuhusu ombi la Sudan la kujiunga na EAC.

Katibu Mkuu wa jumuiya ya Africa mashariki Dk. Richard Sezibera, amesema mazungumzo hayo yatakayohusisha timu ya ngazi ya juu yanatarajiwa kufanyika Alhamisi na Ijumaa wiki hii  katika makao makuu ya jumuiya hiyo jijini Arusha

Amesema mazungumzo hayo yanafuatia kikao cha 27 cha Baraza la Mawaziri la Jumuiya hiyo kilichofanyika Agosti 31 mwaka huu, ambacho kiliidhinisha kufanyika mchakato wa mazungumzo na Sudan Kusini kujiunga na EAC

Mazungumzo hayo yanatarajiwa kuwa katika mifumo mitatu ambayo yatahusisha watalaamu kutoka nchi wanachama na awamu ya pili yatahusu makatibu wakuu watakaopitia mapendekezo yaliyotolewa na timu ya wataalam na kuiwasilisha kwenye vikao vya mawaziri na awamu ya tatu itahusu ngazi ya mawaziri.

WAHAMASISHWA KUTUMIA VYOO BORA ILI KUZUIA MAGONJWA YA MILIPUKO



Na.Edson Raymond
Kata ya mtamaa manispaa ya Singida inakabiliwa na tatizo la ukosefu wa vyoo bora hali inayoweza kusababisha kutokea kwa magonjwa ya miripuko ikiwemo kipindupindu.

Uchunguzi uliofanywa na standard radio katani hapo umebaini kuwa kati ya kaya tano hadi kumi ni kaya moja tu ndiyo yenye choo bora huku kaya nyingine zikiwa zinatumia vyoo visivyo bora na nyingine kutumia vyoo vya majirani au vya taasisi za elimu kama vile shule.

Baadhi ya wakazi walihojiwa na standard radio wamesema kukosekana kwa vyoo bora kumesababishwa na kukosekana kwa elimu huku wengine wakisema vyoo vingi vilibomolewa na mvua zilizonyesha mwanzoni mwa mwaka huu

Akizungumzia tatizo hilo Diwani wa kata hiyo Bw. Gwae Mbua amesema kuwa kwa kuanza wameanza kuweka msisitizo katika shule kuwa na vyoo bora na baada ya kukamilika mpango huo utahamia katika makazi ya wananchi ambapo sheria zimewekwa kwa wale watakao kiuka maagizo ya kuwa na vyoo bora. 

UMASIKINI WA KIPATO KWA WANAMTAMAA WA SINGIDA SASA BASI.


Na.Edson Raymond
Kata ya mtamaa manispaa ya Singida inatarajiwa kuunganishiwa nishati ya umeme wa grid wa taifa kupitia mradi wa umeme vijijini REA ili kukabiliana na umasikini wa kipato kwa wananchi wa kata hiyo.

Mjumbe wa halmashauri kuu ya taifa CCM Bw. Hassan Mazala wakati akizungumza na wananchama wa CCM katika kata hiyo ambapo amesema upembuzi yakinifu juu ya mradi huo unatarajiwa kuanza mwezi huu.

Amesema kuwa endapo umeme ukiunganishwa katika kata hiyo kutasaidia wananchi kujishughulisha na shughuli za kiuchumi ambazo zinategemea nishati hiyo na hatimaye kuondokana na umasikini wa kipato unaowakabili wakazi wa kata hiyo

Aidha Bw Mazala ametoa wito kwa wananchi wa kata hiyo kuwa tayari kuonyesha nia ya kuhitaji huduma hiyo kwa kujiandikisha hali ambayo itaongeza juhudi za mradi huo wa REA kwenda kasi kutokana na mahitaji ya idadi kubwa ya watu.

Tuesday, November 5, 2013

SHERIA YA DAWA ZA KULEVYA KUWA NA MAHAKAMA MAALUM.


 Na.Iman Musigwa
Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Ester Bulaya, ameitaka serikali kufanya mabadiliko ya sheria ya dawa za kulevya na kuanzisha mahakama maalumu ya kushughulikia wahalifu wa dawa hizo

 Amewaslisha maelezo hayo jana kuhusu tatizo sugu la uagizaji, uuzaji na usafirishaji wa dawa hizo ambalo linaloongezeka kwa kasi nchini
Amesema ni wakati mwafaka kwa Bunge na serikali kuona uzito wa tatizo la dawa za kulevya kutokana na ukweli kwamba katika miaka ya karibuni tatizo hilo limeongezeka kwa kasi kubwa hali inayosababisha athari kubwa za kiuchumi
Ripoti mpya ya hivi karibuni ya ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kupambana na Mihadarati na Uhalifu imetamka kwamba Tanzania ni kinara wa kupitisha dawa hizo katika nchi za Afrika Mashariki, na Mkoa wa Tanga kama wa hatari zaidi.

Hata hivyo waziri wa nchi ofisi ya waziri mkuu sera na uratibu wa bunge Bw Wiliamu Lukuvi amesema kauli ya serikali itatolewa kupitia waziri wa katiba  na sheria kuhusu  mikakati ya kutekeleza jambo hilo